Alhamisi 29 Mei 2025 - 20:39
Eneo la Utawala wa Imam Mahdi (a.s.) na Kituo chake

Hawza/ Kuna riwaya nyingi zilizopokelewa ambazo kwa uwazi zinabainisha kwamba utawala wa Imam Mahdi (as) utakuwa wa kidunia.

Shirika la Habari la Hawza - Hakuna shaka kwamba utawala wa Imam Mahdi (as) ni wa kimataifa, kwa sababu Yeye ndiye alie ahidiwa wanadamu wote na ndiye anayetimiza matarajio ya wanadamu wote. Hivyo basi, yale yote ya mazuri na mema yatakayopatikana chini ya utawala wake yataenea duniani kote.

Kuna riwaya nyingi zinazothibitisha kwa uwazi kwamba utawala wa Imam Mahdi (as) utakuwa wa kidunia. Kwa mfano, katika hadithi ya Mtume Mtukufu (saw) imekuja kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:

«... وَ عِزَّتِی وَ جَلَالِی لَأُظْهِرَنَّ بِهِمْ دِینِی وَلَأُعْلِینَّ بِهِمْ کَلِمَتِی وَ لَأُطَهِّرَنَّ الْأَرْضَ بِآخِرِهِمْ مِنْ أَعْدَائِی وَ لَأُمَلِّکَنَّهُ مَشَارِقَ الْأَرْضِ وَمَغَارِبَهَا... .»

Naapa kwa izza na utukufu wangu, hakika nitadhihirisha dini yangu kwao juu ya dini zote, na kwao nitalitukuza neno langu, na kwa wa mwisho wao hakika nitaitakasa ardhi kutoka kwa maadui wangu, na nitamfanya kuwa mtawala wa mashariki na magharibi ya ardhi. (Kamaaluddin, Juzuu ya 1, uk. 256)

Imam Baqir (a.s.) pia amesema:

«اَلْقَائِمُ مِنَّا ... یبْلُغُ سُلْطَانُهُ اَلْمَشْرِقَ وَ اَلْمَغْرِبَ وَ یظْهِرُ اَللَّهُ عَزَّ وَ جَلَّ بِهِ دَینَهُ عَلَی اَلدِّینِ کُلِّهِ وَ لَوْ کَرِهَ اَلْمُشْرِکُونَ فَلاَ یبْقَی فِی اَلْأَرْضِ خَرَابٌ إِلاَّ قَدْ عُمِرَ....»

Qa’im (as) ni kutoka kwetu (Ahlul-Bayt). Ufalme wake utafikia mashariki na magharibi, na Mwenyezi Mungu kwa kupitia yeye ataieneza dini yake juu ya dini zote, hata kama washirikina watachukia. Na hakutakuwa na sehemu yoyote duniani iliyoharibika isipokuwa itajengwa tena. (Kamaaluddin, Juzuu ya 1, uk. 330)

Kituo cha Utawala wa Mahdi (as)

Ama kituo cha utawala wa kimataifa wa Imam Mahdi (as), ni mji wa kihistoria wa Kufa, ambao wakati huo utapanuka kwa kiwango kikubwa sana kiasi kwamba utajumuisha pia mji wa Najaf, uliopo umbali wa kilomita chache kutoka Kufa. Hii ndiyo sababu katika baadhi ya riwaya, "Kufa" na katika nyingine, "Najaf" zimethibitishwa kama makao makuu ya utawala wa Mahdi.

Imam Sadiq (as) amesema katika riwaya ndefu:

«... دَارُ مُلْکِهِ اَلْکُوفَةُ وَ مَجْلِسُ حُکْمِهِ جَامِعُهَا...»

Makao ya utawala wake ni Kufa, na mahali pa hukumu yake ni msikiti wake mkubwa. (Bihar al-Anwar, Juzuu ya 53, uk. 11)

Ni muhimu kueleza kwamba mji wa Kufa, tangu enzi za kale, umekuwa ukiheshimiwa na familia ya Mtume Mtukufu (saw) na ulikuwa kituo cha utawala cha Amir al-Mu’minin Ali (as). Msikiti wake maarufu ni moja kati ya misikiti minne mashuhuri zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam Ali (as) alikuwa akiswali humo, kutoa khutba humo, kuhukumu humo, na hatimaye aliuawa kishahidi kwenye meherabu ya msikiti huo huo.

Utafiti huu unaendelea...

Imenukuliwa kutoka katika kitabu "Negin-e Āfarinish" huku ikifanyiwa baadhi ya marekebisho kiasi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha